SUBSCRIBE TO OUR YOUTUBE CHANNEL-Shec Media.........LIKE OUR FACEBOOK PAGE-Shec Media..... FOLLOW US ON INSTAGRAM-@shecmedia_tz........WHATSAPP NUMBER +255 752 0133 43

Saturday, December 30, 2017

Rwegasira: Ruksa viongozi wa dini kusifia Serikali













Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira amesema viongozi wa dini wakiisifia Serikali
au viongozi wake
hawatakuwa wametenda
kosa lolote.

Ametoa kauli hiyo siku moja baada ya kutoa msimamo wa Serikali kuhusu taasisi za dini, ukiwataka viongozi wake kutojihusisha na masuala ya siasa, bali wajikite kuzungumzia mambo yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao, vinginevyo zitafutwa.

Serikali ilitoa onyo hilo baada ya viongozi wa dini kutumia ibada za Sikukuu ya Krismasi kukosoa baadhi ya mambo yanayoendelea nchini, ikiwamo uhuru wa kutoa maoni na viongozi kukubali kukosolewa.

Akizungumza jana na gazeti hili, Meja Jenerali Rwegasira alisema viongozi wa dini wanapaswa kujikita kuzungumzia masuala ya dini na kuachana na ya kisiasa.

Alipoulizwa iwapo kusifia utendaji kazi wa Serikali na viongozi wake ni kosa alisema, “Mimi sioni kama ni kosa, unapozungumza mambo yanayoleta umoja hakuna kosa ila kukosoa viongozi, kuwakashifu hatuwezi kukubali.”

Mwandishi alipohoji kama kusifia si moja ya mambo ya siasa na linaweza kuleta mvutano alisema, “Ninaloangalia ni je, wanachosema kinaleta mtafaruku katika jamii, lakini kama unazungumza au kuhamasisha amani hilo si tatizo.”

Kuhusu kutofautisha siasa na maisha ya kawaida na hasa kwa viongozi wa dini alisema, “Ujue siasa ni kila mtu anavyoitafsiri, mfano unaweza kuwa unazungumza na watu ukasema uongo, utasikia wanasema hizo siasa sasa.”

Awali, Rwegasira akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Ujerumani Deutsche Welle (DW) kuhusu onyo la Serikali alisema viongozi wa dini wanapaswa kujikita katika masharti ya kuanzishwa kwa taasisi na jumuiya zao na si katika siasa.

“Labda naweza kushindwa kutofautisha kati ya kukosoa Serikali na siasa, ukianza kuingiza siasa katika nyumba za ibada unaanza kuingiza siasa katika nyumba za dini ambazo si kazi zao,” alisema Rwegasira.

“Kazi yao wao ni kueneza dini, kueneza neno la Mungu, si kuingia mambo ya siasa, kushambulia viongozi wa Serikali wanakuwa wamekwenda kinyume cha malengo ya usajili wao. Nashauri na nimewaambia, waachane na mambo ya siasa waende katika dini kwani kuna tatizo gani?

“Kama Serikali inakwenda vibaya watumie majukwaa yao kuzungumza na si kutumia nyumba za ibada yanayounganisha waumini kuzungumza siasa na tulichokifanya sasa ni kuwakumbusha tu na hakuna yeyote aliyechukuliwa hatua,” alisema.

Wakati Serikali ikitoa onyo na ufafanuzi huo, mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe ametofautiana na Serikali akisema viongozi wa dini wanapaswa kuachwa waikosoe. “Kesho tutazitaka taasisi za dini zihamasishe amani, maendeleo, zipongeze ‘Its important’ (ni muhimu) kukubali kukosolewa,” ameandika Bashe katika akaunti ya Twitter.

Alisema Serikali haipaswi kufanya hivyo ikiwa hazivunji sheria. “Taasisi za dini zina haki kutoa maoni yao juu ya siasa, uchumi na masuala yote ya kijamii, viongozi wa dini wana nafasi yao.”

Juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam kuhusu onyo hilo alisema si kweli kwamba wamezuiwa lakini wajaribu kutumia lugha za staha na kutokutoa kauli kamilishi zisizokuwa na ushahidi.

“Wako wazi kusema chochote kwa mujibu wa Katiba za nchi, sheria zetu… anayesema mtu kazuiliwa kuzungumza uhuru wake wa maoni atakuwa na matatizo mengine, ninachokifahamu kuzungumza kauli za matusi ni makosa,” alisema Polepole.

No comments:

Post a Comment